dc.description.abstract | Fonimu ni kipashio kidogo cha sauti ya lugha chenye uwezo wa kubainisha maana na hudhihirika
kama irabu au konsonanti. Kama ilivyo katika lugha nyinginezo ulimwenguni, Kiswahili vilevile
kina fonimu za kategoria mbili yaani irabu na konsonanti. Hata hivyo, idadi ya fonimu konsonanti
za Kiswahili inaelekea kuainishwa tofautitofauti kwa mujibu wa wanaisimu mbalimbali wa
Kiswahili. Mathalani, wanaisimu wengine wanadokeza idadi ya fonimu konsonanti kuwa 24, 25,
26, 29, 32 au 33. Kwa upande mwingine, miundo ya silabi za Kiswahili pia hudokezwa kuwa
tofauti kama vile 4, 5, 6, 7 na 8. Idadi tofauti ya fonimu konsonanti za Kiswahili pamoja na idadi
tofauti ya miundo ya silabi za Kiswahili huelekea kuwakanganya wasomaji wa lugha ya Kiswahili.
Hivyo basi, makala hii inalenga kuhakiki fonimu na miundo mbalimbali ya silabi za Kiswahili. Ili
kufanikisha uhakiki huu, makala hii imehusisha katika upeo wake vijimada kama vile: dhana ya
fonimu, uhakiki wa idadi ya fonimu za Kiswahili pamoja na mifano ya fonimu zenyewe. Makala
imeshughulikia pia dhana ya silabi na uhakiki wa miundo ya silabi za Kiswahili. Uhakiki wa
miundo ya silabi umeshughulikiwa ili kuangazia tofauti zinazodhihirika baina ya wanaisimu wa
Kiswahili kuhusu idadi kamili ya miundo ya silabi za Kiswahili pamoja na mifano inayotolewa.
Katika kujaribu kutanzua mgogoro uliopo, makala imerejelea kanuni zifaazo zinazoweza kutumiwa
na mwanaisimu katika utambuzi wa fonimu na zinazotumiwa pia katika uundaji wa silabi. | en_US |