Mikakati na mitindo katika ujifunzaji wa kiswahili kama lugha ya biashara miongoni mwa wafanyabiashara jijini Kampala-Uganda
Abstract/ Overview
Dhima mojawapo ya lugha ya Kiswahili ni ukuzaji wa sekta ya uchumi. Kiswahili kama lugha ya pili nchini Uganda, kilianzishwa kwa ajili ya kuendeleza biashara na dini. Ujifunzaji na matumizi yake hayajaendelezwa kwa kina. Hata hivyo unapokwenda katika maeneo ya biashara, utakuta Kiswahili kikitumika miongoni mwa wafanyabiashara. Hali ya jinsi wanavyojifunza na kutumia Kiswahili kuendeleza biashara na changamoto wanazokumbana nazo katika matumizi ndilo pengo lililoshughulikiwa katika utafiti huu. Azma ya utafiti huu ilikuwa kuchunguza mikakati na mitindo katika ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya biashara miongoni mwa wafanyabiashara jijini Kampala, Uganda. Madhumuni mahsusi yalikuwa: Kufafanua mikakati na mitindo ya kujifunza Kiswahili kama lugha ya kibiashara jijini Kampala Uganda, kutathmini jinsi mikakati na mitindo mbalimbali huwezesha kujifunza Kiswahili kama lugha ya kibiashara jijini Kampala na kupambanua changamoto zinazokumba wafanyabiashara wakati wa kujifunza Kiswahili kibiashara na kuchanganua mikakati ya namna ya kutatua changamoto zinazowakabidhi wafanyabiashara kujifunza Kiswahili kibiashara. Utafiti huu uliongozwa na kiunzi cha nadharia mbili: Kwanza, Nadharia ya Stephen Krashen (1987) ambayo ina mihimili mitano; nadharia tete ya upataji/ujifunzaji, nadharia tete ya mfumo asili, nadharia tete ya dhana mpya na nadharia tete ya kichujio athari. Pili, Nadharia ya modeli ya elimu ya Richard Gardener (2000). Mihimili iliyohusika ni; mhimili wa jitihada, nia/ari, motisha changamani, uwezo wa kufanikiwa na mwelekeo chanya. Utafiti ulifanyika mjini Kampala nchini, Uganda katika Ekedi ya Mukwano, Simlaw International Limited na soko la Kikuubo. Utafiti ulijikita katika ujifunzaji na ufunzaji wa lugha ya pili na Isimujamii. Utafiti huu ulichanganua mikakati na mitindo ya kujifunza na kutumia lugha ya Kiswahili kibiashara pamoja na changamoto za ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya biashara miongoni mwa wafanyabiashara jijini, Kampala. Usampulishaji dhamirifu ulitumiwa kwa kurejelea aina yake ya usampulishaji mpokezano kifu ambapo uteuzi dabwa dabwa ulitumiwa kuteuwa sampuli ya wasailiwa 260 ya wafanyabiashara kutoka Ekedi ya Mukwano, Simlaw International Limited na soko la Kikuubo. Sampuli kusudio ilitumika kuteua Ekedi 2 na soko Moja la biashara anuwai kuhusika katika utafiti huu. Mbinu za hojaji, usaili na uchuzaji zilitumiwa kukusanya data miongoni mwa wafanyabiashara nyanjani. Vifaa vya utafiti ni pamoja na hojaji, dodoso, mwongozo wa uchunzaji vilitumika kukusanya data nyanjani. Data ilichanganuliwa kutumia mkabala mseto na kuwasilishwa kimaelezo ukishirikisha majedwali. Matokeo ya utafiti yalionyesha kwamba wafanyabiashara walitumia mikakati ya nyimbo/ukariri, mwanafunzi kwa mwanafunzi, matumizi ya lugha chanzi, kuongea, mawasiliano, mitagusano ya ukuruba kati ya wanunuzi na wauzaji, teknolojia, mapango binafsi, utambuzi na urejeleaji. Mitindo ya mwingiliano iliyodhihirika ni dukuduku, kusikiza, ujifunzaji asilia, mwelekeo, hamasa, kuashiria na tabia za mjifunzaji. Hii ilifanyika kupitia kusikiza nyimbo, wafanyabiashara kufundishana wenyewe kwa wenyewe, uhamishaji sheria kutoka lugha chanzi, mawasiliano baina yao na wanunuzi, kutagusana na wajuao Kiswahili, matumizi ya teknolojia, kujipangia namna ya kujifunza, utambuzi, dukuduku, hamasa, mwelekeo, kuashiria na tabia ambazo baadhi ya wafanyabiashara walikuwa nazo. Utafiti huu ulibaini changamoto za kisarufi, muda wa kujifunza, kutumia lugha kimshitukizo, mwelekeo hasi, athari za kisiasa, umri, uoga, tofauti za kijinsia na kanuni za kiisimu. Utafiti huu utachangia katika taaluma ya Isimujamii na ujifunzaji wa lugha ya pili. Utafiti huu ulipendekeza tafiti zaidi kufanyika katika kutambua mikakati na mitindo zaidi katika sekta nyinginezo.